Kati ya watumishi hao 11, waliotuhumiwa katika kadhia hiyo, 10 wamechukuliwa hatua za kinidhamu na mmoja hakupatikana na hatia yoyote. Kati ya hatua hizo ni pamoja na kuvuliwa hadhi, kushushwa vyeo na ngazi ya mshahara na kubadilishwa vituo vya kazi kwa baadhi ya watumishi waliotuhumiwa.
Naibu Waziri wa Fedha, Janeth Mbene alisema hayo jana akijibu maswali ya Mbunge wa Mfenesini, Nassib Suleiman Omar (CCM), kuhusu taarifa za hivi karibuni za kuchotwa kwa Sh bilioni 3.5 kutoka Hazina na baadhi ya maofisa wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wakati Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na Mhasibu Mkuu wakiwa nje ya nchi.
Mbunge huyo alitaka kufahamu utaratibu unaoruhusu maofisa wa ngazi za chini kutoa kiasi kikubwa namna hiyo cha fedha kutoka Hazina; na kama Serikali haioni kuwa utaratibu wa viongozi waandamizi wa wizara kusafiri wote nje ya nchi mara kwa mara na kuacha maofisa wa ngazi za chini ni kukiuka sheria na kuisababishia Serikali hasara kubwa na ni hatua zipi zimechukuliwa dhidi ya wahusika na udhibiti gani umewekwa.
“Napenda kulihakikishia Bunge kuwa hakuna wizi uliotokea katika mchakato wa kuomba na kupokea fedha kwa ajili ya safari ya Rais,” alisema Mbene na kuongeza:
“Baada ya uchunguzi kukamilika, imebainika kuwapo ukiukwaji wa taratibu za kiutawala na kifedha. Kati ya watumishi 11 waliotuhumiwa, watumishi 10 walichukuliwa hatua za kinidhamu na mmoja hakupatikana na hatia. Kati ya hatua hizo ni pamoja na kuvuliwa hadhi, kushushwa vyeo na ngazi ya mshahara na kubadilishwa vituo vya kazi kwa baadhi yao.”
Akijibu swali la nyongeza la Mbunge huyo aliyetaka kuwafahamu watumishi hao na adhabu zao na kama mashauri yao yalifikishwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mahadhi Juma Maalim, alikiri suala hilo kufikishwa Takukuru.
Maalim alisema suala hilo lilishughulikiwa na pande tatu; Takukuru, Ofisi ya Rais na Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, na wahusika wa kashfa hiyo, wote walitoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.
Alisema aliyekuwa Mkuu wa Itifaki, Balozi Anthony Itatiro, alivuliwa cheo cha ubalozi na kuondolewa ukurugenzi, wakati wahasibu waliteremshwa vyeo. Balozi Itatiro alivuliwa wadhifa huo na Rais Kikwete.
Aidha, katika majibu yake kwa swali la msingi, Naibu Waziri wa Fedha alisema maofisa masuhuli ndio wenye mamlaka ya kisheria ya kuidhinisha matumizi makubwa ya fedha katika wizara au taasisi za umma.
Pia alisema sheria, taratibu na kanuni za utumishi wa umma zinaruhusu maofisa waandamizi kukaimu nafasi za viongozi wanapokuwa katika safari za kikazi au likizo