Jumatatu, 29 Julai 2013

RC, RPC Arusha wawakana FBI


Arusha, Habari na MTANZANIA Jumapili,Picha na 2jiachie.
MKANGANYIKO wa taarifa za ushiriki wa Makachero wa Taasisi ya Kijasusi ya Marekani (FBI), katika uchunguzi wa mlipuko wa bomu katika Viwanja vya Soweto, jijini Arusha, sasa umechukua sura mpya,
Ikiwa ni takribani mwezi mmoja na siku 13 tangu mlipuko huo utokee kwenye mkutano wa Chadema wa kufunga kampeni za uchaguzi mdogo wa madiwani, viongozi waliowahi kuthibitisha juu ya ushiriki wa makachero hao wa FBI kwenye uchunguzi wa tukio hilo sasa wameanza kukana matamshi yao.
MTANZANIA Jumapili lilipomtafuta Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas, ambaye mwanzoni mwa mwezi huu alikaririwa na chombo kimoja cha habari (si Mtanzania) akithibitisha ushiriki wa FBI katika upelelezi huo, alikana kuwahi kuzungumza juu ya taarifa hizo.

Juni 12 mwaka huu, gazeti hilo lilimkariri Sabas akisema: “Tunaendelea na uchunguzi wa kina mlipuko wa bomu Soweto, tayari wenzetu wa FBI na polisi wa Kenya wamefika kushirikiana nasi, nachukua fursa hii kuwaomba wenye ushahidi utakaosaidia upelelezi kujitokeza”.
Akizungumza na MTANZANIA Jumapili, Kamanda Sabas alisema, hajawahi kutoa taarifa kama hizo.

“Watu wanatoa wapi hizo taarifa, mimi sijawahi kutoa taarifa hizo,” alisema Kamanda Sabas.

Kuhusu watu waliodaiwa kushikiliwa kutokana na mlipuko huo wa bomu, Kamanda Sabas alisema kwa sasa wapo nje kwa dhamana, kutokana na upelelezi wa tukio kuendelea.

“Ikifikia hatua ya kujulishwa nitawaita kwa sasa bado tunaendelea na uchunguzi,” alisema Kamanda Sabas.

Wakati mkanganyiko huo wa FBI ukionyesha kuchukua sura tofauti, taarifa za vyombo vya habari zimewahi kuunukuu Ubalozi wa Marekani nchini ukikana kuwapo kwa wapelelezi wake jijini Arusha kuchunguza tukio hilo.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magesa Mulongo, ambaye ndiye Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa, alipoulizwa juu ya taarifa za kukanganya za ushiriki wa FBI kwenye tukio hilo la bomu, alijibu kwa kifupi; “Tafuta watu wanaofanana na swali hilo.”

Hata hivyo, Mwandishi wa habari hizi alipomueleza kwamba ameulizwa swali kama Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Arusha, Mulongo alisema; “Hakuna kitu kama hicho.”

Akiwa katika cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa wa Arusha (RCC), Mulongo aliwaambia wajumbe wa kikao hicho kuwa taarifa za awali kutoka kwa makachero wa polisi nchini zimebaini mtandao wa ulipuaji mabomu jijini Arusha, ulipangwa ndani ya jiji hilo.

Mulongo alisema mbinu hizo zilijulikana kutokana na wananchi waliojitokeza kuwasilisha ushahidi kwa vyombo vya dola ambapo mpaka wakati huo ushahidi ulionyesha mtandao wa waliolipua mabomu hayo ulianzia jijini Arusha.

Hivi karibuni, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, alisema kuwa Jeshi la Polisi mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha waliwadanganya Watanzania kuwa Makachero wa FBI wanakuja kuchunguza tukio hilo wakati si kweli na Ubalozi wa Marekani ulikanusha suala hilo.

Mbowe alisema kauli kama hizo zimekuwa zikitumika kuwahadaa Watanzania.

Juni 15, mwaka huu, katika viwanja vya Soweto, CHADEMA wakiwa kwenye mkutano wa kufunga kampeni za uchaguzi mdogo wa madiwani, bomu lililipuka na kuua watu wanne na kujeruhi takribani 70.

Tukio hilo liliibua hisia nyingi na wakati fulani kulazimu maofisa wa Jeshi la Polisi Makao Makuu Dar es Salaam kwenda jijini Arusha kufuatilia kwa kina ambapo baadaye ilielezwa kuwa FBI wametua jijini humo ili kubaini ukweli.

Tangu kutokea kwa mlipuko huo, kumekuwa na mvutano mkubwa baina ya Jeshi la Polisi na Chadema, baada ya Mwenyekiti wa chama hicho kuueleza umma kwamba wanao ushahidi wa polisi kuhusika kwenye tukio hilo, huku akigoma kuwasilisha ushahidi.

Mbali na bomu la Soweto, bomu jingine lilirushwa katika Kanisa la Mtakatifu Joseph Mfanyakazi, Olasiti na kusababisha watu watatu kufariki ambapo upelelezi wake nao unatajwa kuendelea kufanywa.
Habari na MTANZANIA Jumapili