
Idadi kubwa ya watanzania walishiriki
katika maadhimisho hayo hayo ambayo yalianza saa 2:30 asubuhi na
kupambwa na gwaride rasmi lililoandaliwa na vikosi mbalimbali vya ulinzi
na usalama na kupendezeshwa na halaiki ya wanafunzi 2,695 kutoka
Tanzania Bara na Visiwani waliofanya maonyesho mbalimbali ya kuashiria
maadhimisho ya muungano.
Viongozi mbalimbali wakiwamo wastaafu
kutoka Tanzania Bara na Visiwani walishiriki kwenye maadhimisho hayo
ikiwa ni ishara ya kuuenzi na kuulinda muungano huo.
Viongozi hao ni pamoja na Rais wa
Zanzibar, Dk Mohamed Shein, Makamu wa Rais wa Tanzania, Dk Mohamed
Gharib Bilali, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, Makamu wa Kwanza wa Rais
Zanzibar, Maalim Seif Sharrif Hamad na Makamu wa pili wa Rais Zanzibar,
Balozi Seif Idd.
Wengine waliohudhuria maadhimisho
hayo ni Rais mstaafu wa Zanzibar, Aman Abeid Karume, Rais mstaafu wa
awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi, Rais mstaafu wa awamu ya tatu wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Benjamin Mkapa na mawaziri wakuu
wastaafu, Edward Lowassa na Frederick Sumaye.
Baada ya viongozi kuketi katika
nafasi zao, gwaride rasmi lenye gadi kumi lilipita na kutoa heshima zao
mbele ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Baada ya hapo vijana wa halaiki
walionyesha maumbo mbalimbali kuashiria maendeleo yaliyopatikana nchini
kwa muda wa miaka 49 tokea taifa la Tanzania liundwe rasmi kabla ya
Wanahalaiki kujipanga na kuonyesha taswira mbalimbali na kuimba wimbo wa
kuhamasisha kudumisha muungano.
Hata hivyo, baadhi ya viongozi wa upinzani hawakuweza kushiriki kwenye maonyesho hayo.
Viongozi hao ni Mwenyekiti wa Chama
cha NCCR-Mageuzi, James Mbatia, Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe na Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi
(CUF), Profesa Ibrahim Lipumba.
Akizungumza na waandishi wa habari
baada ya kumalizika kwa shughuli za maadhimisho hayo, mjumbe wa Kamati
Kuu Chadema ambaye pia ni Mjumbe wa Tume ya Marekebisho ya Katiba,
Profesa Mwesiga Baregu alisema kuwa, Watanzania wanapaswa kujivunia
Muungano walionao kwa sababu umedumu kwa miaka 49, akieleza kuwa ni
nadra sana kuona nchi za Afrika au Ulaya kuendeleza muungano wenye umri
mkubwa kama huu wa Tanganyika na Zanzibar, hivyo basi wanapaswa kuuenzi
na kuulinda kuendeleza amani iliyopo.
Wakati huohuo, Rais Jakaya Kikwete
ametoa msamaha kwa wafungwa 4,180 waliokuwa wakitumikia vifungo vyao
katika magereza mbalimbali hapa nchini katika kuadhimisha miaka 49 ya
muungano.
Wafungwa waliosamehewa ni
wanaotumikia kifungo kisichozidi miaka mitano, ambapo mpaka siku ya
msamaha yaani April 26, watakuwa wameshatumikia robo ya vifungo vyao,
wafungwa wagonjwa wa Ukimwi, kifua kikuu na kansa ambao wamethibitishwa
na jopo la madaktari.
Pia wazee wenye umri wa miaka sabini
au zaidi, wafungwa wa kike walioingia na mimba gerezani, walioingia na
watoto wanaonyonya na wasionyonya, wakiwamo walemavu.
Msamaha wa Rais pia umeenda kwa
wafungwa walemavu wa mwili na akili na wafungwa ambao hadi siku ya jana
walikuwa wameshakaa gerezani kwa muda wa miaka mitano na wameonyesha
kuwa na tabia nzuri.